Kwa ufupi:
Bonde la Mto Kilombero ni eneo tajiri na lina rutuba tele. Rutuba na wingi wa maji unatokana na kuwa jirani na Misitu ya Milima ya Udzungwa.Mazao makuu katika bonde hili ni miwa, mpunga, mahindi, matunda na mbogamboga.Asilimia kubwa ya ardhi yenye rutuba inalimwa kilimo cha aina moja cha miwa na mashamba ya mpunga. Kwa sababu hii, watu wanalaumu kuwa kuna ukosefu wa ardhi ya kulima mazao mengine, fursa ya kuongeza aina mbalimbali za mazao pamoja na kupanda miti.Licha ya kulima mashamba makubwa ya kilimo cha aina moja, watu wengi wa bonde hili bado wanategemea nishati kuni kwa ajili ya kupikia. Kwa kuwa wananchi wamekatazwa kuingia katika Msitu wa Milima ya Udzungwa, jamii inalazimika kukata miti iliyopo vijijini na misitu jirani kama vile Msitu wa Magombera. Hali hii inachangia uharibifu wa misitu na mazingira kwa ujumla.