Kwa ufupi:
Katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, tatizo la
utapiamlo limekuwa tatizo sugu. Kiwango cha
wanaosumbuliwa na tatizo hili katika nchi yetu kama
asilimia thelatini ya watu wote. Jambo hili si la kufumbia
macho kwa maana nguvu kazi kubwa ya nchi inapotea.
Tatizo hili pia linasababisha watoto wengi mashuleni
kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao. Kwa mantiki
hii maendeleo ya nchi yanafifia kiuchumi na kielimu pia.
Kujikwamua katika tatizo hili sio jambo rahisi. Hata hivyo,
tunaamini kuwa, bila hata msaada kutoka nje ya kaya, kaya
nyingi zinao uwezo wa kujinasua nalo. Kikubwa ambacho
wanakikosa ni taaluma katika kutumia baadhi ya malighafi
waliyo nayo kiutaalamu kuwaondolea kero hii.
Zao la soya limesaidia sehemu nyingi duniani kuondoa
utapiamlo, lakini katika Tanzania zao la soya halijatumika
kikamilifu kwa sababu za kukosa taaluma za namna ya
kulisindika na pia mapishi mbali mbali yanayotokana nalo.
Kijitabu hiki ni juhudi makusudi za wataalamu wachache
walioguswa na hili tatizo na kuamua kuwasaidia wale wengi
wasio na hiyo taaluma kutangaza na kuhamasisha kilimo cha
soya sio tu kwa ajili ya kupunguza utapiamlo na hivyo
kuboresha afya bali pia kutumia zao hili hili kupunguza au
kuondoa umaskini katika kaya. Azma ya juhudi hizi ni kuona
Tanzania nzima ikinufaika na hivyo kupunguza asilimia ya
wenye utapiamlo na maskini katika taifa letu.