Kwa ufupi:
Samaki kama viumbe hai wengine wanahitaji kula chakula ili waishi na kukua. Katika mazingira ya asili kama vile mito, maziwa na bahari, samaki hula chakula cha asili kinachopatikana ndani ya maji. Vyakula hivyo ni pamoja na jamii ya mimea na vijidudu wanaopatikana kwenye maji. Lakini, samaki wa kufugwa hususan ufugaji wa kibiashara, huhitaji kulishwa chakula cha ziada chenye ubora iliyo na virutubisho vinavyohitajika ili aweze kukua vyema na kwa haraka zaidi. Uandaaji wa chakula cha ziada cha samaki hutegemea zaidi aina ya samaki, mfumo wa samaki husika katika kumeng’enya (kusaga) chakula pamoja na kiasi cha virutubisho vinachohitajika.