Kwa ufupi:
Mbegu za maboga zimekuwa kimbilio namba moja kwa baadhi ya watu, wakiwamo kina baba wanaozichangamkia kwa nia ya kujiongezea nguvu za kiume, sawa na ilivyo kwa samaki pweza na supu yake. Madaktari na wataalamu wa lishe wanathibitisha kuwa mbegu za maboga zina kiwango kikubwa cha virutubishi vya vitamin na madini na hivyo kusaidia katika kuupa mwili nguvu na kuukinga dhidi ya maradhi mbalimbali yakiwamo ya baadhi ya aina za saratani, kisukari, moyo na ini. Imeelezwa na wataalamu kuwa kama ilivyo kwa sifa ya mnofu wa pweza, mbegu za maboga pia zina sifa ya kuwa sawa na kifurushi cha madini yanayomfaidisha mlaji kwa wakati mmoja, baadhi ya kiwa ni ya chuma, manganizi, maginizia, zinki na shaba. Walaji wa mnofu wa pweza hunufaika pia kwa wingi wa virutubishi kama protini, mafuta (fats) vitamin B12, selenium, madini ya chuma, shaba na vitamin B6.