Kwa ufupi:
Kutokana na ukweli kwamba muhogo huharibika baada ya siku chache (2-3) baada ya kuvuna ni vyema ukasindikwa ili kuwa katika hali ya kutumika kwa muda mrefu ujao. Sababu nyingine ya kusindika muhogo ni kuongeza thamani ya zao hili, kwa mfano usindikaji huzalisha bidhaa zinazoweza kuwa na mvuto zaidi kwa walaji, mali ghafi kwa ajili ya bidhaa za viwandani na madawa, na upunguzaji wa gharama za usafiri pale ambapo usindikaji unafanyika kweneye maeneo ya uzalishaji. Nyenzo zitumikazo kusindika zao hili hutegemea sana aina ya bidhaa inayokusudiwa.
Ukataji wa chips au silesi waweza kufanywa kwa kutumia nyenzo za asili ambapo kisu kikali na mikono ya binadamu ndiyo vitegemezi. Njia hii inafanywa kwa taratibu sana na hivyo kutokidhi mahitaji makubwa. Kwa mahitaji makubwa kidogo nyenzo zilizotengenezwa viwandani mahususi kwa kazi hii ni muhimu. Iwe njia za asili zimetumika au kwa kutumia nyenzo zilizotengenezwa mahususi kwa usindikaji ni lazima kwanza muhogo uwe umemenywa na kusafishwa kwa maji safi.