Kwa ufupi:
Ndugu wakulima, kupata chakula cha kutosha na kilicho bora kwa kila
mwananchi ni suala gumu ambalo linahitaji mipango na mikakati mizuri
ya serikali kupitia Wizara husika. Matatizo makubwa yanayowakabili
wananchi ni kuchelewa kukamilisha hatua za mwanzo za matayarisho
ya mashamba, kulima eneo kubwa ambalo hawana uwezo nalo na
kutokutumia njia za utaalamu pamoja na pembejeo bora za kilimo.
Ndugu wakulima, moja ya kikwazo kikubwa ni uwezo mdogo wa kutumia
zana bora za kilimo, mbegu bora, mbolea na kutozingatia kanuni na
taaluma bora za uzalishaji ambazo zinatolewa na Wizara ya Kilimo na
Maliasili. Vikwazo hivi humsababishia mkulima kutumia nguvu nyingi,
muda mrefu na kupata mavuno hafifu na tija ndogo.
Ndugu wakulima, kwa miaka mingi neno “Ukulima wa Kisasa”
limekuwa ni wimbo lakini bado mkulima wa visiwani anategemea
zana na pembejeo duni kama vile mbegu na jembe la mkono (kijembe
kongoroka). Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo
na Maliasili inafanya mabadiliko makubwa katika kilimo ili kukifanya
kilimo hicho kiwe katika mfumo wa kisasa “Mapinduzi ya Kilimo”.
Ndugu wakulima, katika kufanikisha suala hili Serikali imeongeza
upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo yakiwemo matrekta
makubwa na madogo, mbegu bora na mbolea, kuongeza usamabazaji
wa taaluma kwa wakulima kwa kuongeza idadi ya mabwana/
mabibishamba katika shehia pamoja na kutoa ruzuku ya aslimia 75%
kwa kazi za utayarishaji wa mashamba na ununuzi wa mbegu bora na
mbolea.
Ndugu wakulima, hatunabudi kuunga mkono juhudi hizi za Serikali
ili kufanikisha azma ya “Mapinduzi ya Kilimo” hivyo tunaipongeza na
tunaiomba iendelee na juhudi zake za kuwashajiisha na kuwashirikisha
wakulima kikamilifu katika kupanga malengo yao juu ya kuendeleza
sekta ya kilimo nchini.
Ndugu wakulima, kwa kuunga mkono juhudi hizi za Serikali, Wizara
ya Kilimo na Maliasili itaendelea kutoa mafunzo ya utumiaji bora wa
zana na pembejeo za kilimo na kuweka mipango maalumu ya mafunzo
kwa kila shehia juu ya umuhimu wa zana hizo pamoja na matumizi
yake ili kufikia lengo la wakulima katika kujitosheleza kwa chakula
na kuimarisha afya za jamii pamoja na kuinua hali zao za maisha na
kuipunguzia mzigo Serikali kwa kuagiza chakula kutoka nje ya nchi