Kwa ufupi:
Kilimo ni nguzo muhimu katika uchumi na maendeleo ya Taifa hususani vijijini na kinachangia zaidi ya asilimia 95 ya mahitaji ya chakula nchini. Sekta
ya Kilimo imeajiri zaidi ya asilimia 78 ya Watanzania wote; na pia inachangia karibu nusu ya pato la Taifa. Hata hivyo, kaya nyingi bado zinazalisha
chakula kwa ajili ya kujikimu tu. Kilimo cha Tanzania kwa sehemu kubwa bado kinategemea mvua, hivyo ni rahisi kuathiriwa na mabadiliko ya
tabianchi. Athari za mabadiliko ya tabianchi tayari zimeanza kujitokeza, ambapo zinarudisha nyuma juhudi za Serikali katika kuongeza tija na
uzalishaji katika Sekta ya kilimo na kuleta athari za muda mrefu iwapo hatua za kukabiliana nazo hazitakuwepo. Hivyo ujumuishaji wa Kilimo
Kinachohimili Mabadiliko ya Tabianchi katika miradi ya maendeleo utasaidia kukuza kilimo na maendeleo ya nchi kwa ujumla.