Kwa ufupi:
Kilimo cha vitunguu maji ni muhimu sana hapa Tanzania. Vitunguu vinaweza kutumika kama
zao la chakula au la biashara kwa aina zote za wakulima, wakubwa na wadogo.
Zao la vitunguu linazalishwa kutokana na mbegu, na miche inakuzwa kwenye kitalu kabla ya
kupandikizwa shambani. Miche inakuwa na ‘kuzaa’ vitunguu. Vitunguu vikikomaa, vinavunwa
na kuuzwa au kuhifadhiwa ghalani.
Wingi na ubora wa mavuno hutegemea; hali ya hewa, aina ya vitunguu, aina ya mbegu bora,
usimamizi wa kilimo bora, uangalizi wakati wa kuvuna, usafirishaji na uhifadhi bora. Mavuno ya
vitunguu kwa ekari bado ni madogo sana hapa nchini (kiasi cha tani nne kwa ekari) na upotevu
wa mazao baada ya kuvuna ni mkubwa (kiasi cha 50% – 80%) kutokana na uhifadhi duni.
Hivyo ukiwa kama mkulima unahitaji utaalamu wa kilimo bora cha vitunguu na njia bora za
kuhifadhi ili kuongeza uzalishaji na kipato.