Kwa ufupi:
Maendeleo vijijini hutegemea sana matumizi ya teknolojia. Kwa
kuwa zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania huishi vijijini kwa
kutegemea shughuli za kilimo, ni wazi basi maendeleo yao
hayawezi kupatikana bila kuendeleza kwanza teknolojia ya kilimo.
Mara baada ya uhuru serikali ya Tanzania iliweka sera ya
kuendeleza matumizi ya zana za kisasa katika kilimo. Mkazo
mkubwa ulikitwa katika usambazaji wa matrekta vijijini. Hatua
hiyo ya serikali haikuweza kuleta mabadiliko kwa wakulima
wengi. Sababu kuu ya kushindwa huko ni uwezo mdogo wa
wakulima kugharamia matunzo na uendeshaji wa matrekta hayo.
Kwa kutambua hilo, mradi wa Uboreshaji wa Matumizi
Endelevu ya Wanyamakazi ulibuniwa chini ya mradi mkuu wa
Uhakika wa Chakula na Pato la Kaya kwa Wakulima
Wadogowadogo (TARP II-SUA). Lengo kuu la mradi huu
lilikuwa ni kuhamasisha na kupanua wigo wa matumizi endelevu
ya wanyamakazi vijijini.