Kwa ufupi:
Mwaka 2008/9 RLDC ilifanya majaribio ya mfumo wa ufugaji wa kuku wa asili kupitia
vikundi vidogo vya wafugaji wa vijijini katika vijiji vya Bupandagila na Mbiti, Wilayani
Bariadi katika Mkoa wa Shinyanga. Huu ni ufugaji wa ushirika unaolenga kusaidia
wazalishaji wadogo wa mazao ya kuku. Utaratibu huu unahusisha mgawanyo wa
kazi katika ufugaji ili kurahisisha na kusaidiana majukumu na gharama.
Lengo kubwa la majaribio haya ilikuwa ni kuona kama mfugaji mmoja angepunguziwa
majukumu yake katika uzalishaji ili kuongeza uwezo wake wa uzalishaji. Vijiji husika
vilifanikiwa kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa kuku watano hadi kufikia kuku mia
moja katika miezi michache. Mafanikio ya mradi huu ndio chachu iliyofanya RLDC
kuona umuhimu wa kufundisha na kudurufu mfumo huu katika maeneo mengine
ya nchi na kuweka wazi kwa watu wengine ambao watakuwa tayari kujihusisha na
ufugaji wa kisasa na kibiashara wa kuku wa asili bila usaidizi wa wafadhili.