Kwa ufupi:
Kaliandra (Calliandra calothyrsus) ni mmea aina ya mikunde wenye asili ya Amerika ya Kati na Mexico. Ulipandwa mara ya kwanza nchini Indonesia kwa ajili ya kivuli katika mashamba ya kahawa, lakini kwa sasa mti huo umeonyesha faida zaidi kwa kutumika kama chakula cha mifugo, kuni na kuhifadhi udongo. Katika nchi nyingi ikiwemo Kenya, Tanzania na Uganda, Kaliandra hutumika kama lishe ya ng’ombe wa maziwa na mifugo wengine. Kaliandra ina kiasi kikubwa cha protini (asilimia ishirini hadi ishirini na tano) na huchanganywa na aina nyingine za majani yenye kiwango kidogo cha protini kama vile matete au majani tembo (Napier kwa Kiingereza) ili kuongeza lishe kwa mifugo, uzalishaji wa maziwa na kiasi cha mafuta katika maziwa.
Ijapokuwa Kaliandra haichavulishwi na nyuki, imekuwa chanzo kikubwa cha asali. Nchini Indonesia, nyuki wameweza kutengeneza kilo elfu moja ya asali kwa mwaka kutoka ekari mbili za shamba iliyopandwa Kaliandra. Faida zingine ni kuboresha uchavushaji wa kahawa na kuni ambazo hukauka vizuri na kuwaka kwa urahisi.