Kwa ufupi:
Upungufu wa wekundu wa damu ni moja ya matatizo sugu ya
utaptamlo yanayoathiri watu na kusababisha vito vingi hapa Tanzania.
Kutokana na takwimu zilizopo Shirika la Chakula na Lishe Tanzania,
inakadiriwa kuwa asilimia 32 ya watu milioni 23 (Sensa ya mwaka
1988) wanaathirika. Wanaoathirika zaidi ni wanawake wajawazito na
watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Takwimu hizo
zinaonyesha kuwa wanawake wajawazito wanaoathirika ni asilimia 80
na watoto chini ya umri wa miaka mitano ni asilimia 45.
Tatizo la upungufu wa wekundu wa damu hutokana na sababu nyingi
zikiwemo ulaji duni yaani kutokula chakula cha mchanganyiko na cha
kutosheleza mahitaji ya mwili. Magonjwa mbalimbali hasa malaria na
minyoo ni chanzo kimojawapo cha tatizo. Vile vile uzazi wa karibu
karibu huchangia upungufu wa wekundu wa damu.
Tatizo la upungufu wa wekundu wa damu hapa nchini limeenea zaidi
sehemu ambazo magonjwa ya safura, malaria na kichocho hujitokeza
kwa wingi.
Kitabu hiki kina lengo la kuwaelimisha na kuwaongezea wataalam wa
ugani na viongozi katika ngazi ya wilaya, kata na kijiji ujuzi, maarifa na
uwezo wa kuelewa chanzo, dalili na athari za upungufu wa wekundu
wa damu katika jamii. Maarifa haya yatawawezesha kuishirikisha jamii
katika kuchunguza, na kupima ukubwa wa tatizo, kufanya uchambuzi
wa kina wa tatizo na kubuni mbinu za kulitatua.
Kitabu kina sura tano. Sura ya kwanza inazungumzia dhana ya
utapiamlo na jinsi inavyotumika katika kuchanganua tatizo la upungufu
wa wekundu wa damu. Sura ya pili inaelezea umuhimu wa madini ya
chuma, vitamini aina ya folic acid na B12 katika mwili wa binadamu na
madhara yatokanayo na upungufu wake. Sura ya tatu inaelezea dalili na
athari za upungufu wa wekundu wa damu. Sura ya nne inaelezea
mbinu za kukabili tatizo la upungufu wa wekundu wa damu na sura ya
tano inaelezea majukumu na wajibu wa jamii katika ngazi mbalimbali