Kwa ufupi:
UTANGULIZI
Kilimo cha bustani kinahusika na uzalishaji wa mazao ya aina ya
mboga, matunda, viungo na mimea ya mapambo. Kilimo cha
bustani ni chanzo cha ajira na pato kwa wakulima na watu
wengine. Mboga na matunda yanatupatia virutubisho vya kujenga,
kutia nguvu na kulinda mwili. Zaidi ya hivyo, mimea ya mapambo
hutumika katika kuremba na kuboresha sehemu za makazi,
majengo, barabara na sehemu zingine za wazi za jumuia. Hii ni
muhimu sana katika swala zima la kuhifadhi mazingira.
Pamoja na umuhimu huo, kilimo cha bustani hakijazingatiwa sana
hapa nchini hasa katika kueneza taaluma yake. Siku zote
kipaumbele kimekuwa kikiwekwa katika kuhimiza kilimo bora cha
mazao ya asili ya biashara na ya chakula kama nafaka.
Jarida hili limetokana na juhudi za mradi wa SUA-TU katika
kueneza taaluma ya kilimo cha bustani katika vijiji vya mkoa wa
Morogoro. Katika baadhi ya vijiji hapa mkoani, taaluma hii ilikuwa
ni ngeni kabisa mradi ulipoanzishwa hapo mwaka 1996. Kwa
ujumla jarida hili linajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa wakulima
wa vijiji vya Changa, Msongozi, Maharaka (Morogoro vijijini),
Katurukila (Kilombero), Kitange I, Kwipapa, Malui na Tindiga
(Kilosa). Sehemu yake ya kwanza ni juu ya uzalishaji wa miche ya
mboga na matunda katika kitalu na utunzaji wake. Sehemu ya pili
na ya tatu zinajihusisha na kilimo cha mboga ikiwa ni pamoja na
uyoga. Sehemu ya mwisho ni juu ya masoko na uuzaji wa mboga
na matunda, swala ambalo ni muhimu katika kumfanya mkulima
afaidike na juhudi zake baada ya kuzalisha.
Tunapenda kutoa shukrani zetu kwa wakulima wote walioshirikiana
na wataalamu wa mradi wa SUA-TU na pia shirika la USAID la
Marekani ambalo ndilo lilikuwa mfadhili mkuu wa mradi