Kwa ufupi:
Kilimo cha bustani kinahusika na uzalishaji wa mazao ya aina ya mboga, matunda, viungo na mimea ya mapambo. Kilimo cha bustani ni chanzo cha ajira na pato kwa wakulima na watu wengine. Mboga na matunda yanatupatia virutubisho vya kujenga, kutia nguvu na kulinda mwili. Zaidi ya hivyo, mimea ya mapambo hutumika katika kuremba na kuboresha sehemu za makazi, majengo, barabara na sehemu zingine za wazi za jumuia. Hii ni
muhimu sana katika swala zima la kuhifadhi mazingira. Pamoja na umuhimu huo, kilimo cha bustani hakijazingatiwa sana hapa nchini hasa katika kueneza taaluma yake. Siku zote kipaumbele kimekuwa kikiwekwa katika kuhimiza kilimo bora cha mazao ya asili ya biashara na ya chakula kama nafaka. Jarida hili limetokana na juhudi za mradi wa SUA-TU katika kueneza taaluma ya kilimo cha bustani katika vijiji vya mkoa wa Morogoro. Katika baadhi ya vijiji hapa mkoani, taaluma hii ilikuwa ni ngeni kabisa mradi ulipoanzishwa hapo mwaka 1996. Kwa ujumla jarida hili linajumuisha mafunzo yaliyotolewa kwa wakulima wa vijiji vya Changa, Msongozi, Maharaka (Morogoro vijijini),
Katurukila (Kilombero), Kitange I, Kwipapa, Malui na Tindiga (Kilosa). Sehemu yake ya kwanza ni juu ya uzalishaji wa miche ya mboga na matunda katika kitalu na utunzaji wake. Sehemu ya pili na ya tatu zinajihusisha na kilimo cha mboga ikiwa ni pamoja na uyoga. Sehemu ya mwisho ni juu ya masoko na uuzaji wa mboga na matunda, swala ambalo ni muhimu katika kumfanya mkulima afaidike na juhudi zake baada ya kuzalisha. Tunapenda kutoa shukrani zetu kwa wakulima wote walioshirikiana na wataalamu wa mradi wa SUA-TU na pia shirika la USAID la Marekani ambalo ndilo lilikuwa mfadhili mkuu wa mradi.