Kwa ufupi:
Unyonyeshaji wa maziwa ya mama una faida nyingi na unachangia kwa kiasi kikubwa, katika afya na maendeleo ya mtoto, pamoja na afya ya mama. Unyonyeshaji unaboresha afya ya mtoto kwa kumpatia chakula kinachohitajika kwa ukuaji na maendeleo yake. Mtoto mwenye hali nzuri ya lishe huweza kupambana na magonjwa kuliko yule mwenye utapiamlo. Ulishaji sahihi huchangia katika kupunguza makali ya ugonjwa hasa maradhi ya kuhara na yale ya njia ya hewa, endapo mtoto ataugua. Kwa muda mrefu, mpango wa kuzuia magonjwa ya kuhara umetambua kuwa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee bila kumpa mtoto hata maji kwa miezi sita ya mwanzo, kunapunguza kwa kiasi kikubwa maambukizo na vifo vitokanavyo na ugonjwa wa kuhara. Pia kuendelea kumnyonyesha na kumpa mtoto chakula cha nyongeza kuanzia miezi 6 hadi miaka 2 au zaidi ni muhimu.