Kwa ufupi:
Sekta ya ufugaji nyuki Tanzania imeendeshwa bila ya kuwa na sera tangu mwaka 1949 wakati ilipoanzishwa rasmi kama idara katika Wizara ya Kilimo. Tangu wakati huo, mwongozo wa kuendeleza na kusimamia rasilimali za nyuki na mimea ya chakula chao umekuwapo kupitia maagizo ya kitaalamu na kiutawala. Madhumuni makuu ya mwongozo huo yalikuwa ni kuufanya ufugaji wa nyuki uwe wa kisasa kwa kuanzisha mizinga ya masanduku, kuongeza uzalishaji wa asali na nta na kuongeza mapato yatokanayo na uuzaji wa asali na nta nchi za nje .
Mabadiliko mengi ya kijamii, kiuchumi na kimazingira yanayotokea pamoja na marekebisho ya sera kuu ya uchumi yaliyotekelezwa nchini, na ongezeko la kujali uhifadhi wa mazingira ili kuleta maendeleo endelevu ya ufugaji nyuki yamepelekea kuundwa kwa Sera ya Ufugaji Nyuki. Sera hii inazingatia nafasi ya ushirikiano na uratibu wa sekta mtambuka ambao utaimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za nyuki na mimea ya chakula chao katika mashamba ya kilimo, misitu na maeneo ya wanyamapori yaliyohifadhiwa.
Rasimu ya sera ya ufugaji nyuki awali ilitayarishwa kama sehemu ya Sera ya Misitu na utayarishaji wa rasimu hii ulihusisha washikadau husika katika warsha tatu tofauti, mikutano mbali mbali ya Idara ya Misitu na Nyuki, Washauri wa Kitaalamu na kikosi maalumu cha utekelezaji. Rasimu ya mwisho ilitayarishwa kwa kuboresha na kuunganisha hoja, mapendekezo na maazimio yaliyopitishwa na warsha hizo tatu na katika mikutano mingine ya kiushauri.
Chanzo kingine muhimu cha habari zilizotumika katika rasimu hii ya mwisho ni Mpango wa Utekelezaji wa Misitu Tanzania (TFAP) ambao unajumuisha Programu ya Taifa ya Ufugaji Nyuki (NBP). Masuala muhimu yanayohusu maendeleo ya sekta ya ufugaji nyuki yaliyokuwamo katika Programu ya Taifa ya Ufugaji Nyuki ambayo yalitayarishwa mwaka 1989 yakiwahusisha washikadau wakuu katika mikutano ya vijiji na warsha za kitaifa, yamejumuishwa katika sera hii. Iliamuliwa kuwa rasimu inayojitegemea ya Sera ya Ufugaji Nyuki iandikwe badala ya kuijumuisha na ile ya Misitu, ili malengo na madhumuni yake yawe bayana na yenye kueleweka. Hii pia inatazamiwa kuwa itawezesha kuzingatiwa kikamilifu kwa masuala ya sekta ya ufugaji nyuki na yale ya sekta mtambuka zenye misingi yake katika ufugaji nyuki na matamko ya sera ambayo ndiyo msingi wa uundaji wa Sheria ya Ufugaji Nyuki. Sheria ya Ufugaji Nyuki itakuwa ndiyo nyenzo kuu ya utekelezaji wa sera hii.