Kwa ufupi:
KWA miaka nenda rudi, kilimo ndiyo kimekuwa uti wa mgongo kwa watu wengi hasa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.Tangu enzi za mababu zetu, kilimo ndiyo kimekuwa njia ya kuhakikisha kaya zinapata mahitaji muhimu, ikiwemo chakula.Kilimo ambacho kimekuwa kikifanyika sana hasa hapa nchini, ni kilimo cha jembe la mkono. Wachache wenye uwezo, wanatumia plau, yale majembe ya kukokotwa na ng’ombe au punda na wengine wamekuwa wakitumia matrekta. Wakati sisi tukihangaika na kilimo cha jembe la mkono, wanasayansi duniani wameendelea kuumiza vichwa namna ya kukifanya kilimo kiwe cha kisasa zaidi, kinachoweza kuzalisha mazao mengi ndani ya muda mfupi na yenye ubora. Ni hapo ndipo teknolojia ya hydrophonics ilipogunduliwa. Kwa mara ya kwanza, teknolojia hii iligunduliwa na mwanasayansi aitwaye William Frederick Gericke aliyekuwa akifundisha katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley nchini Marekani na alianza majaribio yake kwa kulima nyanya, hiyo ilikuwa ni mwaka 1929.