Kwa ufupi:
Ndugu wakulima, kupata chakula cha kutosha na kilicho
bora kwa kila mwananchi ni suala gumu ambalo linahitaji
mipango na mikakati mizuri ya serikali kupitia Wizara
husika. Moja ya tatizo kubwa linalowakabili wananchi ni
kuchelewa kukamilisha hatua za mwanzo za matayarisho ya
mashamba, kulima eneo kubwa ambalo hawana uwezo nalo
na kutokutumia zana na pembejeo bora za kilimo.
Ndugu wakulima, moja ya kikwazo kikubwa ni uwezo mdogo
wa kutumia zana bora za kilimo, mbegu bora, mbolea na
kutozingatia kanuni na taaluma bora za uzalishaji ambazo
zinatolewa na Wizara ya Kilimo na Maliasili. Vikwazo hivi
humsababishia mkulima kutumia nguvu nyingi, muda
mrefu na kupata mavuno hafifu na tija ndogo.
Ndugu wakulima, kwa miaka mingi neno “Ukulima wa
Kisasa” limekuwa ni wimbo lakini bado mkulima wa visiwani
anategemea zana na pembejeo duni kama vile mbegu na
jembe la mkono (kijembe kongoroka). Serikali ya Mapinduzi
ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo na Maliasili inafanya
mabadiliko makubwa katika kilimo ili kukifanya kilimo hicho
kiwe katika mfumo wa kisasa “Mapinduzi ya Kilimo”.
Ndugu wakulima, katika kufanikisha suala hili Serikali
imeongeza upatikanaji wa pembejeo na zana za kilimo
yakiwemo matrekta makubwa na madogo, mbegu bora na
mbolea, kuongeza usamabazaji wa taaluma kwa wakulima
kwa kuongeza idadi ya mabwana/mabibishamba katika
shehia pamoja na kutoa ruzuku ya aslimia 75% kwa kazi za
utayarishaji wa mashamba na ununuzi wa mbegu bora na
mbolea.
Ndugu wakulima, hatunabudi kuunga mkono juhudi hizi
za Serikali ili kufanikisha azma ya “Mapinduzi ya Kilimo”
hivyo tunaipongeza na tunaiomba iendelee na juhudi zake
za kuwashajiisha na kuwashirikisha wakulima kikamilifu
katika kupanga malengo yao juu ya mpango wa utumiaji wa
zana na pembejeo bora za kilimo.
Ndugu wakulima, kwa kuunga mkono juhudi hizi za Serikali,
Wizara ya Kilimo na Maliasili itaendelea kutoa mafunzo ya
utumiaji bora wa zana na pembejeo za kilimo na kuweka
mpango maalumu ya mafunzo kwa kila shehia juu ya
umuhimu wa zana hizo pamoja na matumizi yake ili kufikia
lengo la wakulima katika kujitosheleza kwa chakula, kuinua
hali zao za maisha na kuipunguzia mzigo Serikali wa kuagiza
chakula kutoka nje ya nchi