Kwa ufupi:
Ndugu Wakulima; sote tunakubaliana kwamba kilimo cha umwagiliaji maji
ndio mkombozi wetu kwa ukulima wa mpunga, umuhimu wake umezidi
kuwa mkubwa kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na hali ya hewa
yanayotokea duniani kote, hali inayosababisha kilimo cha kutegemea
mvua kutokuwa cha uhakika na cha matumaini. Hivyo, tunahitaji kujipanga
vyema na kukiimarisha kilimo cha umwagiliaji maji ili tuwe na uhakika wa
chakula na kupunguza uagizaji.
Kwa mujibu wa Mpango Mkuu wa Umwagiliaji maji wa mwaka 2003,
Zanzibar tunalo eneo la ekari 21,300 ambazo zinafaa kwa kilimo cha
umwagiliaji maji. Hadi sasa eneo lililojengwa miundombinu ni ekari 1,750
sawa na asilimia 8% tu ya eneo lote. Eneo lililobaki lenye ukubwa wa ekari
19,550 kati ya hizo ekari 200 zimejengwa makinga maji, ekari zilizobaki
19,350 zinaendelea kutumika kwa uzalishaji wa mpunga wa kutegemea
mvua.
Ndugu Wakulima pamoja na hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa miundombinu,
bado tunakabiliwa na changamoto za gharama kubwa za ujenzi wa
miundombinu, ukarabati wa visima na pampu kutokana na teknolojia
duni upungufu wa wataalamu na elimu ya uendeshaji wa jumuiya za
wakulima na upungufu mkubwa wa mitaji, utegemezi mkubwa wa nishati
ya umeme, uharibifu wa vianzio vya maji pamoja na ukosefu wa zana
maalum za utayarishaji wa ardhi. Kutokana na changamoto hizo hadi sasa
zaidi ya asilimia 90 ya eneo linalofaa kwa umwagiliaji maji linalimwa kwa
kutegemea mvua hali ambayo inapelekea uzalishaji na tija ndogo.
Ndugu Wakulima, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo 2011 – 2016 Wizara
ya Kilimo na Maliasili imekusudia kuutekeleza kikamilifu Mpango Mkuu wa
Umwagiliaji maji ambao unatarajiwa kutatua changamoto zote za kilimo
hicho. Wizara imezungumza na Serikali ya Korea kupitia Benki ya EXIM –
ambao wamekamilisha uhakiki wa eneo la ekari 5250 ambalo litajengwa
mindombinu ya umwagiliaji maji. Serikali ya Japan na Benki ya BADEA pia
wameonesha nia ya kutusaidia katika Kilimo cha umwagiliaji maji.
Ndugu Wakulima, Wizara imekusudia kuendeleza ujenzi wa miundombinu
na utunzaji wa vianzio vya maji ili sekta ya umwagiliaji maji ipate
maendeleo endelevu na kuwawezesha wakulima kuongeza tija na
uzalishaji wa zao la mpunga. Kuzijengea uwezo Jumuiya za Wakulima wa
umwagiliaji maji ziweze kushiriki kikamilifu katika uendeshaji na utunzaji
wa miundombinu, uhifadhi wa vianzio vya maji na utoaji wa huduma za
Kilimo. Wizara inaendelea kuwashajihisha wananchi kushiriki kikamilifu
katika kuchagua miradi ya kijamii ya umwagiliaji maji ikiwemo ujenzi wa
miundombinu na makinga maji kila wanapopata fursa ya usaidizi wa
Washirika wa Maendeleo.
Ndugu Wakulima, napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wakulima
wa mpunga wa umwagiliaji maji watumie mbegu bora na pembejeo
zinazotolewa na Wizara ya Kilimo na Maliasili ili kuongeza tija na uzalishaji
wa zao hilo na kuhakikisha kuwa miundombinu ya umwagiliaji maji
iliyojengwa kwa gharama kubwa tunaitumia kikamilifu katika uzaalishaji
wa zao hili.