Kwa ufupi:
Korosho ni zao la biashara linaloweza kudumu kwa muda mrefu. Mti wa mkorosho huanza
kutoa mavuno ifikapo miaka mitatu hadi minne baada ya kupandwa. Kadri umri wa
mkorosho unavyo ongezeka, ndivyo mavuno yanavyoongezeka ya. Kiwango cha juu cha
mavuno hupatikana mkorosho unapofikia umri wa miaka saba hadi 10, na baada ya miaka 10
mavuno huanza kupungua.
Mti wa mkorosho huhitaji eneo la kutosha ili kuruhusu ustawi na kuongeza kiwango cha
mavuno. Mti wa mkorosho hustawi zaidi ukanda wa joto. Mikoa inayozalisha zaidi korosho
ni Mtwara, Lindi, Pwani, Tanga, na Ruvuma. Kutokana na tafiti mbalimbali zilizofanywa na
vituo vya utafiti ikiwamo Naliendele, mikoa mingine inayofaa kwa uzalishaji ni Morogoro,
Singida, Iringa, Dodoma na Mbeya.
Zao la korosho lina faida nyingi, zikiwemo; hutumika kama chakula na kuzuia mmomonyoko
wa udongo, na malighafi ya viwandani kwani korosho ni chanzo cha mafuta inapopogolewa.
Vile vile zao la korosho ni chanzo cha ajira cha kuongeza kipato kwa mkulima, hivyo
kumwezesha kuboresha maisha, mfano kujenga nyumba bora na kusomesha watoto na
kinaongeza pato la taifa kwani ni chanzo cha pesa za kigeni
Kijitabu hiki kimeandaliwa kwa ajili ya kumsaidia mkulima kuweza kufahamu kuhusu
namna ya uzalishaji bora wa korosho kuanzia zikiwa shambani mpaka sokoni, ili kuweza
kufikia matarajio yaliyo bora katika uzalishaji wa zao hilo. Hivyo ni matarajio yetu kuwa,
kupitia kijitabu hiki, mkulima wa zao la korosho ataweza kutambua mbinu bora za uzalishaji
wa zao la korosho.