Kwa ufupi:
Wasiwasi unatanda kuhusu uendelevu wa muda mrefu wa sekta ya kilimo. Ardhi yenye rutuba
na maji ya kutosha ni muhimu kwa ajili ya kuendeleza kilimo na kaya. Hata hivyo, katika bara la
Afrika uzalishaji unaotokana na ardhi umekuwa ukiendelea kupungua kutokana na shughuli
za kilimo kilichoshadidi zinazosababisha uharibifu wa ardhi.
Sababu kubwa za uharibifu wa ardhi ni taratibu za kilimo zisizokuwa endelevu kama vile
kulima kwenye miteremko mikali bila ya kuchukua hatua za kuhifadhi udongo na maji, kulima
zao la aina moja tu, utifuaji wa ardhi uliopitiliza, kupungua kwa mazoea ya kupumzisha ardhi
bila ya kuchukua hatua stahiki za kurudishia virutubisho vya ardhi, kuchoma mabaki ya mazao,
kugeuza misitu na vichaka kuwa maeneo ya kilimo cha kudumu, au matumizi yaliyopitiliza
ya misitu kwa ajili ya kuvuna kuni na mbao, mifugo mingi katika eneo dogo la malisho, na
kutokuwepo kwa udhibiti imara wa mboji kwenye udongo.