Kwa ufupi:
Wote tunaiona wazi: watu wameongezeka, miji imekua,
mifugo imeongezeka, mashamba mengi zaidi ....
Vilevile uharibifu zaidi wa ardhi, uharibifu wa misitu,
mmomonyoko wa udongo .... Migogoro mingi zaidi kati
ya wakulima na wafugaji, wachimba madini na wafugaji,
wanyamapori na watu ....
Mahitaji yetu ya kutumia ardhi yanaongezeka wakati
wote, lakini eneo la ardhi haliongezeki. Tutafanyaje ili
tuwe na matumizi mazuri na ya kuridhisha ya ardhi
tuliyonayo, katika mazingira ya hali ya tabianchi na
maliasili, pamoja na tamaduni zetu, njia tunazotumia
kumudu maisha, matarajio na ndoto za jamii yetu?
Kujibu swali hili ndilo lengo la kupanga matumizi
ya ardhi. Na kwa sababu ardhi ni ya msingi kwa jamii,
mpango wa matumizi ya ardhi unakuwa bora pale tu
jamii inaposhiriki kikamilifu kwenye mchakato. Hapo
ndipo linapokamilika suala la “ushirikishwaji” kwenye
mpango shirikishi wa matumizi ya ardhi, yaani LUP.