Kwa ufupi:
Kikundi cha wakulima ni chombo muhimu katika jamii, kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuleta mabadiliko ya kiuchumi hasa pale vinapoanzishwa kwa kuzingatia sheria na
taratibu ambazo wanavikundi wamejiwekea. Mafanikio huwa makubwa zaidi kama wanakikundi hushiriki katika kupanga na kutoa maamuzi ya jinsi ya kuendesha shughuli za kikundi tokea hatua za mwanzo. Kwa kufanya hivyo, na hivyo uwezekano wa kutekeleza yale waliyojipangia huongezeka. Kikundi cha wakulima huanzishwa na kuendeshwa kwa kuzingatia katiba ya kikundi, ambayo hutoa miongozo na maelekezo mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha vikundi vinakuwa ni vyombo imara na hai kiuchumi. Aidha uanzishaji wa kikundi hulenga kuwapa uwezo na kuwawezesha wanachama kutekeleza madhumuni waliyojiwekea katika kuboresha hali zao za maisha. Kikundi cha wakulima kinaweza kuanzishwa mahali popote ambapo pana watu walio katika eneo moja linalowawezesha kufanya shughuli zao za pamoja kwa urahisi na ambao wataonesha nia yao kwa kulipa viingilio na hisa. Idadi ya chini ya watu wanaotakiwa kuanzisha kikundi ni kumi. Hata hivyo, idadi pekee haitoshelezi bali la msingi zaidi ni uhai wa kiuchumi.