Kwa ufupi:
Ili lengo la mradi la kusaidia vijiji kutekeleza mpango wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu kwa Jamii litimie, Mradi unaendelea kupanua elimu na kusaidia vijiji vingine 2 (Ndole na Magunga) kuanzisha misitu ya Hifadhi ya Kijiji na pia kijiji kingine cha Diburuma kilipata elimu na uamasishwaji wa usimamizi wa misitu ya jamii.
Sheria ya msitu ya mwaka 2002 inatoa fursa nyingi kwa jamii kusimamia na kulinda misitu
Sheria inasema kuwa miongoni mwa malengo yake makuu ni kuwapa wajibu na haki
ya kusimamia misitu wananchi ndani na kandokando ya misitu
Wanajamii walielimishwa kwamba wakiweza kutunza misitu yao watapata motisha kama:
❖ Kubaki na 100% ya mapato yatokanayo na mauzo ya mazao ya misitu.
❖ Kubaki na tozo na faini. Faini inayotozwa katika ardhi ya kijiji kutokana na Misitu ya Hifadhi ya Kijiji au Misitu ya jamii inabaki kijijini ili mradi imeelezwa kwenye sheria ndogo za kijiji.
❖ Utaifishaji wa mazao ya misitu na vifaa kutokana na uvunaji haramu.
❖ Wanaweza kufanya uvunaji endelevu wa mazao ya misitu ili mradi imeelezewa kwenye mpango wa uvunaji wa kijiji
Baada ya kuelimishwa wanavijiji wa vijiji vya Ndole, Diburuma na Magunga walianza mchakato wa kusimamia Misitu ya Hifadhi yaVijiji.Vijiji vyote vitatu viliunda kamati ya maliasili ya kijiji yenye wajumbe 12 ikijumuisha wanaume na wanawake. Vijiji vya Magunga na Ndole walifanikiwa kutenga maeneo ya Misitu. Ndole hekta 1,238.81 na Magunga hekta 1,277.3, pia waliandaa mpango wa usimamizi wa misitu, sheria ndogo na kuidhinishwa na Mkutano mkuu wa kijiji na kupelekwa kwenye Halmashauri ya Wilaya kwa idhini na kwaajili ya kusajiliwa kwenye daftari la usajili wa misitu ya vijiji.
Hii inapelekea kufanya jumla ya hekta 10,131.22 kwa vijiji 8 (Bwage, Mziha, Difinga, Msolokelo, Masimba, Makuyu Magunga na Ndole) ambavyo vinatekeleza Usimamizi Shirikishi wa Misitu kwa Jamii na kuidhinishwa na mkutano mkuu wa kijiji. Kwa kipindi cha mwaka 2015 mpango wa usimamizi wa misitu na sheria ndogo za vijiji 3 (Makuyu, Msolokelo na Masimba) zimeidhinishwa na Halmashauri yaWilaya ya Mvomero na kusajiliwa kwenye daftari la usajili wa misitu ya vijiji.