Kwa ufupi:
La Via Campesina na Afrika Kontakt tunakiri kuwa tuko nyuma sana katika kukabiliana na tatizo linalotukabili la mabadiliko ya tabianchi. Sehemu kubwa ya tatizo bado haijatatuliwa, ambayo ni mifumo yetu ya kiulimwengu ya masuala ya kijamii na kiuchumi inayosababisha mabadiliko ya tabianchi. Kwahiyo, lazima tupambane kuhakikisha kuwa mifumo hiyo inabadilishwa. Zaidi ya hapo, tunatakiwa kushiriki katika mchakato mzima wa kutafuta njia na mikakati mbadala ya kuleta mabadiliko halisi. Wakati wa mkutano wa Mazingira wa Paris yaani COP21, wanaharakati wa masuala ya tabianchi walikuwa wakipaza sauti zao kuhusu mabadiliko ya mfumo, na siyo mabadiliko ya tabianchi. Wengi wa wanaharakati hao hapo awali walikuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi. Wanaharakati hao huliona suala la mabadiliko ya tabianchi kama jambo halisi na ambalo hutokea kila siku. Kwa mujibu wa maelezo yao, hatutakiwi kuwasubiri wanasiasa kuchukua hatua, na badala yake wamekuwa wakichukua hatua ambazo kwa bahati mbaya zimekuwa zikipuuzwa na wanasiasa wengi na watunga sera au wamekuwa wakidharauliwa na mfumo.
Lengo la kitabu hiki cha mwongozo ni kuonyesha athari za mabadiliko ya tabianchi zinazowakabili wakulima wadogo, lakini pia kugusia suluhisho ambazo wanaweza kuzitumia kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mwongozo huu umeandaliwa kwa kuzingatia maarifa ya wakulima wadogo kutoka Uganda, Tanzania, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, na Msumbiji. Kutokana na ukweli kuwa jamii za zilizoko katika nchi hizo wanategemea sana mazingira asilia na maliasili zake, wamekuwa wahanga wakubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi. Lakini uhusiano wao wa karibu na mazingira umewesha uwepo wa maarifa kutoka kizazi kimoja hadi kingine ambayo yanatumika kukabiliana na janga la mabadiliko ya tabianchi. Hali iliyopo sasa kwenye majadiliano ya kimataifa kuhusiana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na madhara makubwa ya mabadiliko ya tabianchi vinahitaji kuchukuliwa hatua za dharura. Kwa sasa tunaelewa fika kuwa mfumo wa uzalishaji uliosababisha mabadiliko ya tabianchi hauwezi kutumika kukabiliana na tatizo ambalo wenyewe ulisababisha. Badala yake tunatakiwa kufungua macho yetu ili tuweze kutambua njia zilizopo na tuweze kuziendeleza na kuzitanua ili zisaidie katika mapambano. Hili linajumuisha mabadiliko kwenye mfumo wa uzalishaji wa dunia nzima.