Kwa ufupi:
Sekta ya kilimo inategemewa kama nguzo muhimu ya uchumi nchini Tanzania. Hii sekta inajumuisha uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi na inatoa ajira kwa zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania; na huchangia takribani asilimia 95 ya mahitaji ya chakula kwa Taifa na nusu ya pato la Taifa. Hata hivyo, kilimo hutegemea sana hali ya hewa hasa mvua, hivyo huathirika na athari za mabadiliko ya tabianchi. Athari hizo zinaonekana kwa mifumo tofauti katika sehemu mbalimbali nchini, hivyo kuathiri uzalishaji katika sekta ya kilimo
Katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, sekta ya kilimo imeandaa mwongozo wa kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2017. Mwongozo huu unaainisha mbinu na teknolojia mbalimbali za kuwaongoza watunga sera na watoa maamuzi, maafisa ugani, wakulima, wafugaji na wavuvi katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika kuwasaidia wakulima kuzielewa na kuzitekeleza mbinu na teknolojia mbalimbali zilizoainishwa kwenye Mwongozo, Wizara imeandaa kijarida hiki ambacho kinaainisha baadhi ya mbinu na teknolojia zinazohusiana na mifugo, kilimo na uvuvi. Mwongozo wa kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi umelenga kuonyesha jinsi njia hizo zinavyoweza kufanyika, faida zake na maeneo ambapo zinaweza kutumika ili kuwa na kilimo endelevu, chenye kuongeza kipato na kuleta usalama wa chakula.
Hivyo Mkulima anashauriwa kuwasiliana na afisa ugani aliye karibu naye kwa maelezo zaidi juu ya matumizi ya njia hizi katika eneo husika.