Kwa ufupi:
Misitu ni rasilimali muhimu sana ambayo nchi yetu imejaliwa. Inakadiriwa
Tanzania ina misitu yenye ukubwa wa hekta milioni 48.1 ambayo ni sawa
na asilimia 38 ya eneo lote la ardhi ya nchi yetu. Misitu hii hata hivyo
inakabiliwa na upoteaji wa kiwango cha eneo la hekta 400,000 kwa
mwaka, na hii inasababishwa na kilimo cha kuhama hama, mifugo, moto
na uvunaji holela na usio endelevu wa mazao ya misitu na shughuli
zingine za kibinadamu.
Kutokana na changamoto zinazoikabili misitu na jamii inayoishi
pembezoni mwa misitu, jamii imeamua kuandaa majumuisho ya
changamoto hizo na mapendekezo ya namna ya utatuzi wake. Lengo
ni kutumia fursa ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 katika utatuzi wa
changamoto za misitu na jamii ili misitu yetu iendelee kutoa huduma ya
kiikolojia, kiuchumi na kijamii kwa muda mrefu.