Kwa ufupi:
Hifadhi ya Asili ya Amani ilitangazwa kisheria na Serikali ya Tanzania
katika gazeti la serikali mwaka 1997, ikiwa na lengo la kuihifadhi
bayoanuwai ya Milima ya Usamabara Mashariki. Safu ya Mashariki ya
Milima ya Usambara imeorodheshwa kama kituo cha kimataifa cha
bayoanuwai ya mimea na inajivunia kuwa ya pili kwa kuwa na aina
nyingi za mimea katika bara la Afrika. Pia ilitangazwa na UNESCO
kuwa Hifadhi ya Binadamu na Viumbe hai, mwaka 2000. Hifadhi hii
ya viumbe hai yenye eneo la takribani hekta 83,600 inajumuisha
misitu ya mvua na ardhi ya nyasi na miti ya uwanda wa chini. Ina sifa
ya kuwa na mimea mingi iliyo katika hatari ya kutoweka (ikiwemo
mimea mingi ya madawa) na ni makazi ya zaidi ya aina kumi na tatu
za ndege wasiopatikana mahali pengine. Pia misitu hii mikuu hutoa
maji kwa wakazi zaidi ya 300,000 katika mji wa Tanga, na wenyeji wa
milimani wanategemea misitu hii kwa ajili ya shughuli mbalimbali
za kimaisha.