Kwa ufupi:
Nchini Tanzania, mpango wa matumizi bora ya ardhi vijijini
ulirasimishwa miaka ya hivi karibuni ikiwa ni moja ya mikakati
katika mchakato wa kuleta maendeleo endelevu vijijini.
Utekelezaji wa mpango huu hauna budi kuwa mikononi
mwa wanavijiji wenyewe kwa kiasi kikubwa katika kugawa
ardhi yao kwa matumizi mbalimbali ya kujikimu kimaisha
kwa sasa na siku za baadaye na kuwa na uhifadhi endelevu
wa mazingira. Maendeleo endelevu katika Wilaya ya Mbarali
mkoani Mbeya yanaathiriwa na migogoro ya matumizi ya
rasilimali ardhi na maji kwa muda mrefu sasa. Hii imetokana
na uwezo wa ardhi kupungua kutoa mavuno ya kutosha
na uhaba wa maji kwa matumizi mbalimbali hususan
umwagiliaji, unyweshaji mifugo, uendelevu wa miminiko
la maji kwenye bwawa la umeme, uhifadhi ya bionuai
na mazingira. Mpango wa matumizi bora ya ardhi vijijini
unasaidia kusimamia na utatuzi wa migogoro ya matumizi
ya ardhi, maji na hifadhi ya mazingira.