Kwa ufupi:
Mradi wa Kuongeza Teknolojia za Kupunguza Hewa ya Ukaa na Kuboresha Maisha
ya Jamii zinazozunguka misitu ni sehemu ya Mradi wa Kuweka Mikakati ya Kuokoa Misitu iliyo hatarinini kutoweka nchini Tanzania yaani ‘Strategic Interventions’. Mradi huu upo chini ya Programu ya Kudhibiti na Kukabiliana Mabadiliko ya Tabia ya Nchi Tanzania unaotambuliwa kwa kiingereza kama ‘Climate Change Impact Adaptation and Mitigation (CCIAM) Programme in Tanzania’ unaoratibiwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Morogoro. Mradi huu unavishirikisha vyuo vikuu vitatu nchini Tanzania ambavyo ni Chuo kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo kikuu cha Ardhi (ARU) pamoja na mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA). Pia mradi unavihusisha vyuo vikuu nchini Norway chini ya uratibu wa Chuo kikuu cha Sayansi cha Norway (UMB).
Madhumuni ya Mradi wa Kuongeza Teknolojia za Kupunguza Hewa ya ukaa
na Kuboresha Maisha ya Jamii zinazozunguka misitu ni kusaidia juhudi za
jamii (watu) husika katika kutekeleza hatua mbalimbali za kulinda, kurejesha
na usimamizi endelevu wa misitu ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya
tabia ya nchi. Mradi huu umepangwa kutekelezwa katika Mji Mdogo wa Masasi,
Wilayani Masasi.
Mji mdogo wa Masasi una eneo la kilometa za mraba 376.7 na idadi ya watu ni
zaidi ya 101,059 (kwa mwaka 2007) ambao wanaoishi katika kata sita za mji
huo. Ukiondoa kata ya Mkuti, kata tano zilizosalia ambazo ni Sita, Temeke,
Migongo, Jida na Mtandi zinazunguka Msitu wa Hifadhi wa Milima ya Masasi
ambao ni msitu wa asili. Mnamo tarehe 15 – 22 Mei 2011 timu ya wataalamu
watano wa mradi walitembelea mji huo kwa madhumuni ya kufanya upembuzi
wa awali ndani ya msitu na kufanya mikutano na wadau mbalimbali kama vile
wafanyakazi wa mji ndogo, vikundi vya mazingira na serikali za kata za Temeke,
Migongo na Mtandi kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi huo.
Upembuzi huo wa awali ulibaini kwamba Msitu huo wa hifadhi wa milima
ya Masasi ulikuwa umeharibiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli za
binadamu kama vile kukata miti kwa ajili ya kuchoma mkaa, mbao na kuni, kulima ndani ya msitu na kuchoma moto. Maeneo mengi ya msitu yalikuwa yameathirika ikiwemo kupungua kwa vyanzo vya maji na vyanzo vya maji vilivyosalia maji yake yalikuwa machafu na hayatoshelezi mahitaji ya jamii inayozunguka msitu.
Shughuli za uharibifu wa msitu ziliendelea kufanyika na watu wengi wanaoishi kwenye kata zinazozunguka msitu waliendelea kutegemea rasilimali za msitu
huo ili kujipatia mahitaji mbalimbali yakiwemo maji na mazao mbalimbali.