Kwa ufupi:
Utapiamlo ni miongoni mwa matatizo makubwa ya kiafya ambayo yanaathiri watoto chini ya miaka mitano, wajawazito na wanaonyonyesha, kutokana na mahitaji yao kilishe kuwa makubwa. Licha ya jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, mamilioni ya watoto na kinamama wanaendelea kupata matatizo yatokanayo na lishe duni yakiwemo, uzito mdogo, udumavu, ukondefu, upungufu wa vitamini A, upungufu wa madini joto na upungufu wa wekundu wa damu (anemia).
Utapiamlo husababisha ukuaji duni kimwili na kiakili na vifo vingi miongoni mwa watoto wadogo nchini Tanzania. Huchangia kwa kiasi kikubwa kuongezeka kwa umaskini katika jamii, kwani hupunguza nguvu kazi kutokana na magonjwa, hivyo hupelekea kupungua kwa uzalishaji mali. Sababu ya karibu inayosababisha utapiamlo nchini ni ulaji duni na maradhi. Sababu zilizojificha ni pamoja na upungufu wa uhakika wa chakula katika kaya, upungufu katika utunzaji wa makundi maalum mfano; watoto, wajawazito, nk. na upungufu wa huduma za kimsingi za binadamu mfano elimu, afya, maji, nk. Sababu za msingi ni elimu duni; mfumo wa siasa, itikadi na uchumi; mila na desturi. Kwa sasa jitihada za kutatua matatizo ya lishe nchini zimeelekezwa zaidi katika sekta ya afya, zikijumuisha chanjo, utoaji madawa na virutubishi katika vyakula.
Zipo njia nyingine za kutatua tatizo la utapiamlo kama utumiaji wa vyakula vyenye virutubishi mbalimbali na elimu ya lishe lakini bado havijatiliwa mkazo unao stahili. Kuna uhitaji wa sekta mbalimbali kushirikiana katika kutatua tatizo la utapiamlo.
Mwongozo huu umetengenezwa kuwawezesha walimu wa shule za msingi na watumishi katika ngazi ya jamii kutumia elimu ya lishe kupitia vyakula katika kutatua tatizo la utapiamlo. Chakula kitakachopewa kipaumbele katika Mwongozo huu ni viazi vitamu na bidhaa zake.
Viazi vya rangi ya chungwa, hutumika kuondoa tatizo la upungufu wa vitamini A na vitamini nyingine pamoja na utapiamlo. Viazi vitamu vyote vina viinilishe vya vitamini C, E, K, pamoja na kundi la vitamini B, lakini viazi vya rangi ya chungwa vina vitamini A zaidi. Kulingana na tafiti zilizofanyika, kiasi cha gramu 125 (nusu kikombe cha chai) za viazi vilivyochomwa au kuokwa zina uwezo wa kukidhi mahitaji ya vitamini A ya watoto na kinamama ambao wanamahitaji makubwa ya kimwili ya vitamini A kwa siku. Matumizi ya viazi vya rangi ya chungwa na majani yake kutaimarisha lishe na usalama wa chakula katika kaya na pia kunaweza kuzalisha kipato cha ziada katika kaya.