Kwa ufupi:
Tume kupitia Ushirika imefanikiwa kuboresha maisha ya wananchi kupitia shughuli wanazozifanya zinazowaingizia kipato kwa muunganiko wa Ushirika. Kwa mfano, wakulima wameweza kulipwa fedha zao za mazao kwa uharaka baada ya kuuza mazao yao kupitia Mfumo wa Stakabadhi za Ghala. Tume imeendelea kufanya Usimamizi thabiti wa Vyama vya Ushirika ambao umechangia kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la Pato la Taifa. Mfano, kati ya mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022 jumla ya Tani 9,804,347 za mazao ya kimkakati ziliuzwa kupitia Vyama vya Ushirika, na jumla ya Shilingi 2,917,816,152,983.61 zililipwa kwa wakulima.
Vilevile, Serikali inakusanya tozo na kodi mbalimbali kupitia Mamlaka zake zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Vyama vya ushirika. Mfano, Serikali katika mwaka 2021/2022 ilipokea jumla ya Shilingi 15,144,077,319.16 zikiwa ni fedha za ushuru unaotokana na zao la korosho uliolipwa na vyama vya TANECU, MAMCU, RUNALI, LINDI MWAMBAO, TAMCU na CORECU. Vilevile, jumla ya Shilingi 1,041,957,051.00 zimepokelewa kama ushuru kutoka katika Vyama vya Ushirika vya KDCU na KCU kupitia zao la kahawa.
Viwanda Vidogo, vya Kati na Vikubwa 279 vimeanzishwa nchini kupitia Mfumo wa Uendeshaji wa Vyama vya Ushirika. Katika Msimu wa 2022/2023 Vyama Vya Ushirika vilitumia jumla ya Shillingi 397,706,245,786 kununua pembejeo za kilimo kwa ajili ya wakulima wa zao la Korosho, Kahawa, Tumbaku na Pamba. Tume pia kupitia Vyama vya Ushirika imeendelea kuratibu masoko na biashara ya zao la Ufuta nchini ambapo katika msimu wa 2022/2023 jumla ya kilo 79,170,426 zenye thamani ya Shilingi 245,130,400,328.00 zimeuzwa kupitia ushirika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na Songwe na kuwezesha Halmashauri zake kupata ushuru wa zao wenye thamani ya Shilling 6,022,450,313.00
Tume vilevile inasimamia Vyama vya Ushirika vya Kifedha (SACCOS) ambapo hadi kufikia mwaka 2021 kabla ya kuanza kutekeleza Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha kulikuwa na SACCOS 3,831 zenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.6 na Akiba ya Shilingi Bilioni 803 pamoja na Amana za Shilingi Bilioni 149.2. Baada ya usajili mpya kwa mujibu wa Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha, hadi kufikia mwezi Novemba, 2022 kuna jumla ya SACCOS 743 zenye wanachama 1,731,237 wenye Amana za Shilingi Bilioni 713.6, Mali za Shilingi Bilioni 945.3 na Hisa zenye thamani ya Shilingi Bilioni 149.2.
Kutokana na mafanikio yanayopatikana, Vyama vya Ushirika chini ya usimamizi wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika vinafanya kazi nzuri ya kukuza kipato na uchumi wa wananchi. Kwa hiyo, Watanzania walioko katika sekta zote wanaendelea kuhimizwa kujiunga katika Vyama vya Ushirika ili waweze kuinua uchumi wao na wa Taifa kwa ujumla.
Endelea kupata elimu, habari na matukio mbalimbali ya Ushirika kupitia Jarida hili.
Karibu sana