Kwa ufupi:
Maelfu ya wakulima walionufaika na mpango wa ruzuku ya mbolea kwa msimu wa 2022/2023 wana hadithi ndefu ya kuwasimulia wenzao ambao hawakubahatika kujiunga na mpango huo.
Mpango huu wa ruzuku ya mbolea umebuniwa na serikali ili kuimarisha sekta ya kilimo na kuchochea ongezeko la pato la taifa na hatimaye kuwatajirisha wakulima ambao kwa miongo mingi walishindwa kupiga hatua za maana katika ustawi wao.
Katika Tanzania zimepita kampeni nyingi zilizolenga kuimarisha kilimo tangu kupatikana kwa uhuru zaidi ya miaka 60 iliyopita. Nyingi ya kampeni hizo zilifanikiwa kuleta hamasa miongoni mwa wakulima ili waongeze tija katika uzalishaji wa mazao mbalimbali. Hata hivyo, kwa bahati mbaya kampeni hizo hazikuwa endelevu kiasi cha kuwakwamua wakulima waondokane na umaskini.
Ndiyo maana katika kukifanya kilimo chetu kiwe endelevu na kilete tija kwa wakulima serikali imebuni mpango huu wa ruzuku ya mbolea ili kuzalisha chakula kwa wingi na kupata malighafi viwandani kwa bidhaa zitokanazo na juhudi za wakulima wanaounda uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.
Ni jambo la kutia moyo kwamba baada ya kubaini mafanikio yatokanayo na mpango huu wa ruzuku ya mbolea kwa msimu wa 2022/2023 serikali kwa kauli moja imeamua kuuendeleza kwa misimu mingine “kuanzia 2023/2024 hadi 2025/2026.” Sasa hivi kinachosuburiwa ni maelekezo ya serikali jinsi mpango huu utakavyotekelezwa kwa misimu hiyo miwili.
Nia ya serikali ni kuwawezesha mamilioni ya wakulima wazidi kunufaika na ruzuku ya mbolea ili kuchochea kukua kwa uchumi wa taifa. Vyama vya ushirika vilivyozagaa nchi nzima ni lazima vijipange kikamilifu katika utekelezaji wa mpango huu huko vijijini.
Ni jukumu la serikali za mitaa huko vijiijini zisaidie usimamizi wa bei elekezi ya mbolea kwa kila kituo kutegemeana na mazingira halisi ya sehemu inayohusika. Tunatarajia kwamba vituo vya mauzo ya mbolea vikiwa karibu na wakulima, kundi hilo la wachapa kazi wa Tanzania litahamasika zaidi katika kutumia mbolea ili kukuza uzalishaji.
Kampeni hii ya ruzuku ya mbolea ni lazima iote mizizi katika ngazi zote kuanzia vitongoji, vijiji, kata na tarafa – maeneo ambayo kuna idadi kubwa ya wananchi. Viongozi wa ngazi zote kuanzia vijiji hadi taifa ni lazima wasimame kidete kuhakikisha kampeni hii inafanikiwa kwa sababu imebuniwa kumkomboa mkulima wa Tanzania katika karne hii inayoshuhudia maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia.
Miaka ya mwanzo ya uhuru, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, altuasa kutimiza wajibu wetu ili kujiletea maendeleo. Kwa sasa hamasa hii ni lazima ihamie kwa wakulima kwa kuwataka wajisajili kwa wingi ili waweze kufaidi matunda ya ruzuku ya mbolea. Kwa njia hiyo watakuwa wanapiga vita umaskini na kubadili hali zao za maisha.
Ni vizuri kwa Watanzania kuchangamkia fursa kama hizi zinazotolewa na serikali ambazo zinalenga kubadili maisha yao baada ya miongo mingi ya kuelea kwenye dimbwi la umaskini.