Kwa ufupi:
Aina nyingi za mafuta ya kula yanayotumika hapa nchini hutokana na mazao ya mbegu
za mafuta, mbata na michikichi. Mafuta hupatikana baada ya kusindika mbegu au
mbata. Mafuta hutumika kama kiungo muhimu katika mapishi mbalimbali kwani huongeza
ladha ya chakula. Mafuta pia ni muhimu kwa afya, huongeza joto na nguvu mwilini.
Uzalishaji wa mazao ya mbegu za mafuta nchini hautoshelezi mahitaji ya viwanda na
kusababisha pengo lililopo kuzibwa kwa kuagiza mafuta toka nje ya nchi. Aidha uzalishaji mdogo wa mazao hayo, umesababisha viwanda vikubwa vya kusindika mafuta nchini kuwa vichache. Uzalishaji mdogo wa mazao haya umetokana na wakulima wengi kutozingatia kanuni za kilimo bora kama vile kupanda aina ya mbegu zenye kutoa mafuta mengi, jambo ambalo linafanya bidhaa ipatikanayo kutokana na mazao hayo kuwa kidogo na kutotosheleza mahitaji ya walaji. Wakulima wengi hutegemea kuuza mazao ya mbegu za mafuta kwa wasindikaji wadogo wanaotumia mashine ndogo ndogo zilizosambaa katika maeneo mengi yanayozalisha mazao hayo. Vilevile teknolojia za usindikaji za asili zinazoendelea kutumika katika maeneo mengi, husababisha upotevu wa mafuta wakati wa usindikaji kwani mafuta mengi hubakia kwenye mashudu. Lengo la uandaaji wa kitabu hiki ni kuelimisha jamii kuhusu hifadhi, usindikaji na matumizi ya baadhi ya mazao ya mbegu za mafuta baada ya kuvuna ili kuongeza usalama wa chakula pamoja na kipato. Walengwa wa kitabu hiki ni wakulima na wadau wengine ambao hujiajiri katika sekta ya kilimo Teknolojia zilizoanishwa katika kitabu hiki pia zitasaidia wasindikaji wadogo wa mazao ya mbegu za mafuta kupata uwezo wa kuchagua na kutumia mashine zenye ufanisi mzuri ili kuweza kukamua kiasi kikubwa cha mafuta kutoka kwenye mbegu na
kupunguza upotevu wa bidhaa.