Kwa ufupi:
Mihogo, viazi vitamu na viazi mviringo ni mazao muhimu ya mizizi nchini Tanzania. Mazao hayo ni chanzo cha virutubishi mbalimbali hususan wanga, vitamini A (viazi vitamu vya rangi ya karoti), vitamini B na protini (majani ya mihogo). Mazao ya mizizi hustawi katika sehemu nyingi nchini na yana sifa ya kustahimili hali ya ukame hasa mihogo na viazi vitamu. Mazao hayo yana matumizi mengi kama vile chakula cha binadamu, mifugo, katika viwanda ni mali ghafi katika utengenezaji wa karatasi, wanga, gundi na katika utengenezaji wa vyakula maalum vya mchanganyiko wa mazao kwa lengo la kuboresha virutubishi. Mazao ya mizizi huharibika haraka yakihifadhiwa katika hali ya ubichi kutokana na kuwa na maji mengi. Hali hii pia husababisha usafirishaji kwenda kwenye masoko ya mbali kuwa mgumu. Aidha, matumizi ya mbinu duni wakati wa kuvuna, kutayarisha,
kufungasha na kusindika husababisha upotevu mkubwa wa mazao hayo hadi kufikia aslimia 45. Ili kupunguza upotevu wa mazao ya mizizi, Wizara ya Kilimo na Chakula imetoa kitabu hiki kuwa mwongozo wa kuwelimisha wakulima na wadau wengine matumizi ya mbinu bora za uvunaji, utayarishaji, usindikaji, ufungashaji na hifadhi ya mazao ya mizizi baada ya kuvuna. W akulima na wadaun wengine wakizingatia matumizi ya teknolojia zilizoainishwa, wataweza kupunguza upotevu wa mazao ya mizizi, kuongeza akiba ya chakula, kuongeza thamani, matumizi ya mazao hayo na kujiongezea kipato hivyo kupunguza umaskini.