Kwa ufupi:
Licha ya kutumia kiwango cha kisasa cha teknolojia husika, utunzaji fanisi baada ya kuvuna ni jambo muhimu katika kufikia lengo linalokusudiwa. Wakati wazalishaji wa kiwango kikubwa wananufaika kwa utumiaji wa tekinolojia za kisasa za baada ya kuvuna kwa kuwekeza katika mitambo ya hali ya juu, siyo rahisi kwa wazalishaji wa kiwango kidogo kufanya hivyo, badala yake teknolojia rahisi na za gharama ndogo zinaweza
kuwafaa. Wazalishaji wa kiwango kidogo ni walio na mitaji midogo, wakulima wanaouza mazao moja kwa moja sokoni na wafanyabiashara wa kati wanaowauzia mazao wasafirishaji wa nje ya nchi. Mambo mapya yaliyovumbuliwa hivi karibuni katika teknolojia zinazotumika baada ya kuvuna (mazao) yanajibu matamanio ya kuepuka matumizi ya gharama kubwa za utendaji kazi na kupata bidhaa bora. Njia hizi zinaweza zisiwe endelevu kwa kipindi kirefu kutokana na masuala ya kijamii na kiuchumi, kiutamaduni na au mazingira. Kwa mfano, matumizi ya viuatilifu baada ya kuvuna yanaweza kupunguza matukio ya mashambulizi ya wadudu waharibifu lakini yanaweza kuwa na matokeo yenye gharama kifedha na katika mazingira. Pamoja na hayo, kuongezeka kwa mahitaji ya matunda na mboga zinazozalishwa kwa kutumia kilimo hai/kilimo ogani, kunatoa
fursa ya upatikanaji wa soko kwa wakulima wa kiwango kidogo na wauzaji. Hali halisi ya wanaohudumia (handlers) mazao kwa kiwango kidogo inajumuisha matumizi ya
nguvu kazi ya ziada, ukosefu wa mikopo kwa ajili ya kuwekeza katika teknolojia zinazotumika baada ya kuvuna, nishati ya umeme isiyoaminika, ukosefu wa usafiri mbadala, vifaa vya kuhifadhi na au vifungashio na kuwepo kwa vikwazo vingine. Kwa bahati nzuri, kuna wigo mpana wa teknolojia rahisi za kutumia zinazoweza kuchaguliwa na mbinu nyingi zenye uwezo wa kukidhi mahitaji muhimu ya watunzaji wa kiwango kidogo na wauzaji wa mazao. Kwa miaka mingi mbinu zilizopo katika mwongozo huu, zimefanikiwa kupunguza upotevu na kutunza ubora wa mazao ya bustani katika sehemu mbalimbali duniani.